Pol
isi wakiwa wameweka ukuta kwenye lango kuu la Kuingilia jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani, jijini Dar es Salaam jana, ili kuzuia kundi la waumini wa dini ya Kiislamu, waliokuwa wameandamana kushinikiza wenzao waliokamatwa kwa kushawishi waislamu kukataa kuandikishwa Sensa waachiwe huru.
BAADHI ya waumini wa dini ya Kiislamu kutoka misikiti mbalimbali ya Dar es Salaam, jana walifanya maandamano ya amani bila kibali, katikati ya Jiji na kuvuruga kwa muda mfumo wa mawasiliano katika mitaa kadhaa, ukiwamo wa Ohio ambao Polisi walilazimika kuufunga.
Mitaa mingine iliyofungwa kwa muda kutokana na maandamano hayo ni Maktaba, Posta, Sokoine, Morogoro, Bibi Titi, Samora na Ali Hassan Mwinyi.
Tukio hilo lililotokea saa nane mchana, lilisababisha msongamano wa magari katika kipindi chote ambacho waumini hao walikuwa katika ofisi za Wizara ya Mambo walikoenda kushinikiza wenzao waliokamatwa kwa kugomea Sensa waachiwe.
Maandamano hayo yalihitimishwa kwa kuweka kambi katika ofisi hizo ambako waliteua wajumbe waliozungumza na uongozi wa wizara hiyo.
Katika maandamano hayo, waumini hao walikuwa na mabango yanayopinga Sensa, kuishutumu Serikali na taasisi zake kwa madai kuwa haki zao zinakiukwa.
Walikusanyika kwa wingi mbele ya ofisi hizo kwenye makutano ya Mitaa ya Ohio na Maktaba, baada ya kuzuiwa na polisi kuingia ndani.
Mkusanyiko huo uliwalazimu polisi kuweka kamba nzito ya wigo na kuwaamuru waandamanaji hao wasivuke jambo ambalo Waislamu hao walilitii, lakini wakiendelea kutoa maneno makali kutokana na kile walichodai kuwa ni kutotendewa haki.
Ujumbe uliotumwa ndani uliporejea uliwatangazia wenzao kuwa Serikali imekubali kuwaachia wenzao bila masharti.
Akisoma makubaliano baina ya wizara hiyo na wawakilishi wa waumini hao nje ya ofisi hizo jana, Kiongozi wa Wanafunzi wa Kiislamu, Jaffar Mkene alisema wamekubaliana hivyo kimsingi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbaraka Abdulwakil ambaye walijadiliana naye kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi.
“Ndugu Waislamu wenzangu nasoma mkataba wa makubaliano ambayo tumefikia baina yetu na Serikali,” alisema na kuongeza kuwa wamekubaliana kuwa kuanzia muda huo Waislamu wote ambao wametiwa ndani kutokana na kukaidi Sensa wataachiwa huru.
Kauli hiyo ilipokewa kwa kelele na sauti ya “Takbir!….” kutoka kwa waumini.
Mkene alisema kuwa baada ya kukubaliana katika hilo, hivi sasa nguvu zao wanazielekeza Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) akisema watalala katika ofisi hizo hadi Serikali itakapotamka kwamba imemwondoa Mkurugenzi wake, Dk Joyce Ndarichako.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu huyo wa Mambo ya Ndani ilisema kwamba watuhumiwa hao wameachiwa lakini kwa dhamana.
Awali, mmoja wa viongozi wa waumini hao, Juma Bungo alisema kwamba makubaliano yao yalifanikiwa kwa asilimia 95. Baada ya tangazo hilo waumini hao waliondoka na kuelekea Msikiti wa Kichangani, Magomeni.
No comments:
Post a Comment