Wednesday, November 28, 2012

CECAFA LEO PATAMU KILIMANJARO STARS USO KWA USO NA BURUNDI

 TIMU ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' leo itashuka dimbani kuikabiri Burundi kwa lengo moja la kushinda na kujihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Namboole, Kampala.

Pambano hilo linalotarajiwa kuwa na upinzani mkali litafanyika kuanzia saa 12 jioni, huku likitanguliwa na mechi ya mapema baina ya Somalia na Sudan litakalovurumishwa mnamo saa 10 jioni.



Stars iliyoko katika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu katika kundi B, kama itashinda mchezo huo itafikisha pointi sita na kujiweka vizuri kwenye harakati zake za kusaka ubingwa wa michuano hiyo msimu huu.

Timu hizo zitaingia uwanjani zikiwa katika hali ya kujiamini kufuatia matokeo mazuri ya mechi zilizopita, ambapo Stars iliibanjua Sudan mabao 2-0, huku Burundi ikishusha kipigo cha mbwa mwizi kwa Somalia cha mabao 5-1.

Rekodi ya viwango vya Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA)  vinaweza kuipa jeuri Burundi ambayo iko kwenye nafasi ya 122  na kuiacha Tanzania katika nafasi ya 130, ingawa kiwango cha juu ilichokionyesha Stars katika mechi dhidi ya Sudan kinaipa matumaini Stars ya kuingia uwanjani ikiwa na kiburi.

Katika pambano hilo la leo, mchuano mkali unatarajiwa kuonekana kati ya mshambuliaji wa Stars, John Bocco na nyota wa zamani wa Simba, Selemani Ndikumana wa Burundi ambao katika mechi za timu za mwanzo kila mmoja alipachika mabao mawili.

Washambuliaji hao ni miongoni mwa wachezaji watatu wanaoongoza katika chati ya ufungaji, mwingine akiwa ni Yusuph Ndikumana ambaye pia ana mabao mawili aliyopachika wakati Burundi iliposhinda mabao 5-1 dhidi ya Somalia.

Kocha wa Stars, Kim Poulsen alisema jana kuwa mikakati yake  ya kuimaliza Burundi imekamilika na sasa anasubiri muda tu utimie ili atekeleze mikakati yake.

"Tumejipanga vizuri kuiua Burundi ingawa tunafahamu kwamba tutakabiliwa na upinzani wa hali ya juu,"alisema Kim mara baada ya mazoezi ya asubuhi.

Naye kocha wa Burundi, Lotfy Mohamed alisisitiza kuwa analifahamu vizuri soka la Tanzania hivyo hakuna kitakachomkwamisha asichukue pointi tatu.

"Tanzania tumecheza nayo mara nyingi tu hivyo siwahofii kabisa tupo tayari kupambana na kushinda mchezo pia,"alisema Mohamed.

Sudan Kusini waaga

Wageni Sudan Kusini wamekuwa wa kwanza kuanga mashindano ya Chalenji baada ya jana kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Kenya katika mchezo wa Kundi A.

Sudan Kusini iliyoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu ilipojitangazia uhuru wake kutoka kwa Sudan, ilifungwa bao la kwanza katika dakika 14 na David Ochieng aliyemaliza kona ya Kelvin Omond.

Clifton Miheso aliifungia Kenya bao la pili katika dakika 72, baada ya kupokea pasi nzuri ya Humphrey Mieno matokeo yalimaliza ndoto ya vijana wa Juba kubaki kwenye michuano hiyo baada ya kufungwa mchezo wa kwanza na Ethiopia 1-0.

Wakati huohuo; Kocha wa timu ya Rwanda 'Amavubi', Milutin Sredojovic  'Micho' amesema amefurahia kupata ushindi
katika nchi ambayo alianzia kazi ya ukocha alipotua Afrika.

Amavubi ikiwa chini ya Micho iliidungua Malawi mabao 2-0 katika pambano la michuano ya Chalenji lililopigwa juzi kwenye
dimba la Namboole.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Micho alisema ushindi alioupata umemfanya akumbuke mambo mengi
aliyowahi kuyafanya wakati akiishi nchini Uganda.

"Hii ni nchi ambayo nilianza kufundisha soka nilipofika Afrika kwa mara ya kwanza, nimefurahi kurejea hapa na ushindi, kwa kweli imenifanya nikumbuke mambo mengi sana,"alisema Micho na kuongeza:

"Ushindi huu ni mwanzo tu wafanikio ya baadaye ya Rwanda, kikosi kinachocheza michuano hii ni matunda ya kile kilichoshiriki mwaka jana michuano ya Kombe la Dunia kwa Vijana chini ya miaka 17."
 all the best kilimanjaro stars


No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...